UNATARAJIA NINI KUTOKA KWA MCHUMBA WAKO...?

 
Je, ni kweli kwamba ndoa ni furaha tu? Hakuna huzuni? Hakuna ugomvi? Rafiki zangu, hata viongozi wa dini, wanapofungisha ndoa, husisitiza kuhusu kuvumiliana, kutunzana na kupendana kwa dhati hata katika kipindi cha shida na raha.



Kwa bahati mbaya, baada ya rafiki zetu wanapokea tofauti maneno haya, wanaamini kwa kuambiwa, humaanisha kwamba kupendana labda hata kama fedha ya kula itakosekana nyumbani, mwenzake akiumwa n.k. Huo ni mtazamo tasa. Katika mada hii nitakufumbua, ujue nini zaidi utakutana nacho ukiwa ndani ya ndoa.



KWANINI TUNAJADILI?

Rafiki yangu ipo haja ya kujadiliana juu ya jambo hili tena kirafiki kabisa. Haya ni mambo ambayo sisi vijana tunakutana nayo. Ni wazi kwamba, kila kijana anawaza kuhusu ndoa.



Anawaza kuoa au kuolewa. Anatamani kuwa na familia yake ili aitwe mama au baba, au siyo jamani? Sasa kabla ya kuingia kwenye hizo ndoa ni lazima tuzijue kwanza, hii ndiyo sababu hasa iliyonisukuma kuandika mada hii.



FIKRA ZA WENGI

Kama nilivyoeleza hapo juu, fikra za wengi ni tofauti. Asilimia kubwa wanafikiria zaidi kuhusu maisha mazuri yasiyo na mikwaruzano. Wanawaza kufurahia ndoa na kudhani hakuna changamoto nyingine.

Wapo wanaofikiria hata suala la tendo la ndoa. Kwamba watakuwa huru kukutana kila siku kadiri watakavyoweza kwa kuwa wapo pamoja ndani. Hii ni mitazamo mibaya sana katika ndoa.



Ni kweli unaweza kufanya tendo la ndoa na mwenzako mara nyingi uwezavyo, lakini nani amekudanganya kwamba kila siku utaendelea kumuona kama umuonavyo leo? Amini usiamini, zipo ndoa nyingi zinazolalamikia suala la tendo la ndoa.

Kuna ambao wanadai hawatoshelezwi huku wengine wakilalama kuwa wenzi wao hawataki kabisa kutoa unyumba. Unajua kwa nini? Ama ana mtu mwingine pembeni au amechoshwa na mapenzi ya aina moja kila siku.



(i) Wanaume

Hawa fikra zao huwa kwenye suala la usafi, wanaamini wakiwa kwenye ndoa nyumba itakuwa safi, nguo zitafuliwa, kupikiwa na mambo mengine ya kifamilia.

Akili zao zinakomea hapo tu, hawawazi kuhusu migogoro na namna ya kutatua. Wanaota kuwa na maisha mazuri, kuwa na watoto na kujijengea heshima kwa jamii. Hilo tu, basi!



(ii) Wanawake

Baadhi ya hawa ninaowazungumzia hufikiria kuhusu kuvaa vizuri, kutolewa out, kupata watoto na mengineyo. Kamwe hawana muda wa kufikiria juu ya matatizo ambayo yanaweza kutokea katika maisha ya ndoa.

Hili ni tatizo. Rafiki zangu, maisha ya ndoa hayana furaha siku zote. Kuna wakati dhoruba hutokea na kusababisha mifarakano hivyo kuhitajika umakini wa hali ya juu katika kumaliza tatizo. Si kila siku kuna amani.



TATIZO LIPO WAPI?

Kwa wale ambao wana mitazamo ambayo nimeeleza hapo juu, huwa hawana muda kwanza wa kuwachunguza wapenzi wao, lakini pia wao wenyewe kuonesha tabia zao halisi ili wenzi wao waweze kusoma kama wataweza kuendana nao.

Rafiki zangu, kwa ujumla hatutakiwi kufikiria mazuri pekee kwenye ndoa, kuna mengi ya kuvumiliana. Lakini pia kabla ya kuamua kuingia kwenye ndoa na mwenzako, kipengele kifuatacho hapa chini ni silaha muhimu sana kwako.



ISHI MAISHA YAKO HALISI

Huwezi kumjua mwenzako kama atakuwa anaishi kisanii na wewe. Sikiliza, kwa wiki mnakutana mara mbili tu, tena mnakaa kwa muda usiozidi masaa mawili, si rahisi sana kuweza kujuana tabia zenu halisi.



Pamoja na hayo, wataalamu wa mambo ya mapenzi wanashauri ili mwenzi aweze kuwa wazi zaidi kwa mwenzake ni vyema yeye akaanza kuwa wazi na kuishi maisha yake halisi kwa uwazi. Usijilazimishe kupenda kitu ambacho hukipendi. Kama kuna jambo ambalo analifanya na linakuboa, mwambie ajue ukweli.



Kwanza, uwazi wako kwake utamfanya naye awe wazi kwako. Hatakuwa na sababu ya kuigiza maisha wakati wewe unaishi maisha yako halisi.



Kila mmoja akimjua mwenzake, ndoa haiwezi kuwa na matatizo, maana kila mtu atakuwa anajua anaishi na mtu wa aina gani. Inawezekana kabisa, mmoja wenu akaona tabia za mwenzake zimemshinda. Kama ni kweli na umegundua kwamba kuingia kwenye ndoa ni sawa na utumwa, fanya maamuzi!



NATAMANI sana kuona maisha ya vijana wa sasa yakiwa hayana migogoro, hasa ya mapenzi. Ni furaha yangu kuona vijana wakifanikiwa katika kazi zao na maisha yao kwa ujumla. Rafiki zangu, maisha bora au utaratibu mzuri wa maisha unatokana na uhusiano mwema wa mhusika na mwenzake.



Kama ulikuwa hujui, leo chukua hii elimu, kijana/mtu ambaye amegombana na mpenzi wake usiku uliopita, siku yake huwa nzito sana kazini. Kila anachokifanya hukumbuka ugomvi wa usiku.



Kama mtu ataondoka nyumbani akiwa hana maelewano na familia yake, ni wazi kwamba siku yake itatawaliwa na giza. Hata kama atajitahidi kuficha, lakini itafikia mahali atashindwa. Kazi inahitaji utulivu.



Ndivyo ilivyo katika maisha, lazima upate mwenzi sahihi ambaye atakupa furaha badala ya mateso. Hapa ndipo tunapojadili jambo moja kubwa na muhimu sana; amani na furaha ya ndoa.



Je, wewe unatarajia nini kwenye ndoa yako ijayo? Unahitaji mafanikio au kuvurunda kila siku kwenye biashara zako? Kama unataka kuwa bora, lazima pia uwe na mwenzi sahihi. Rafiki zangu wengi wanajiandaa kwa mazuri tu kwenye ndoa zao.

Hawana mpango na changamoto na migogoro, hapo watakuwa wanakosea sana.



Kama mnakumbuka vizuri, wiki iliyopita nilieleza kwanza sababu za kujadili mada hii, namna ambavyo baadhi ya watu wanawaza na tatizo lilipo, ambapo imeonekana wengi wanaishi na wapenzi wao kabla ya ndoa, maisha ya kuigiza tu! Yaani anaonesha tabia za ‘kupaka rangi’ lakini akishaingia ndani anabadilika.



Kitu kikubwa ambacho nilikifafanua wiki iliyopita ni tabia ya kuishi maisha yako halisi bila kuigiza. Kufanya hivyo kutampa nafasi mpenzi wako naye aishi maisha yake ya kawaida, mwisho kila mmoja atamjua mwenzake.





KEMEA MAPEMA MATATIZO

Katika kuishi kwako maisha yako halisi, mwenzako naye atakuwa kama wewe. Hiyo ni hatua nzuri maana itakuwa rahisi sana kwako kugundua tabia za mwenzako. Hapo utazijua nzuri na mbaya.



Acha kulea matatizo, bila kujali jinsi, mwambie mpenzi wako tabia ambazo hazikufurahishi. Ili aweze kubadilika kwa urahisi zaidi, unatakiwa kumwambia kwa utaratibu, lakini pia umpe sababu za wewe kukataa tabia zake hizo.



Akiendelea nazo kuwa mkali, wakati mwingine ukali unasaidia. Kwa kukemea, kama ni kweli anakupenda na anahitaji uhusiano wenu uendelee, basi lazima atabadilika. Akifanya hivyo itakuwa vizuri zaidi kwako, maana utakuwa na uhakika angalau kwa asilimia chache kwamba mpenzi wako anakusikiliza.



TABIA ZA ASILI

Rafiki zangu, lazima ufahamu kwamba wakati unapambana na tabia za mpenzi wako zisizokupendeza, zipo tabia nyingine ni za asili. Hazibadiliki. Sasa hapo lazima uwe makini kwa mambo mawili; Mosi, zitakuathiri?



Pili, ni tabia zitakazokugombanisha na jamii? Maana kuna tabia nyingine zinavumilika, lakini je, hazitaleta athari kwa majirani zenu watarajiwa? Haya ni mambo ya kuyatafakari kabla ya kuingia kwenye ndoa.



Mathalani, kuna baadhi ya watu wana viburi au dharau za kuzaliwa! Hata umfanyeje, habadiliki. Unaweza kumwuliza kitu akanyamaza. Ni tabia ya kiburi, lakini kwa sababu amezaliwa akiwa na tabia hiyo, hawezi kuiacha. Sasa hapo lazima ujiulize, utawezana naye?

Utaweza kumvumilia na kiburi chake kwa maisha yenu yote? Huu ni mfano tu rafiki zangu, zipo tabia nyingi za asili, ambazo kwa nafasi yako unaweza kuzichunguza kwa mpenzi wako kabla ya kuchukua uamuzi mzito wa kuingia kwenye ndoa.



KUWA MKWELI

Ukweli ni silaha, ni haki na siku zote humfanya mtu awe huru. Kama kuna jambo ambalo hujalipenda kwa mpenzi wako, haraka mwambie. Acha kukaa na vitu moyoni. Si utaratibu mzuri.



Hata kama nguo zake hazikufurahishi mwambie: “Baby yaani kiukweli ukivaa hizo jeans zako hupendezi kabisa. Nadhani uanze kuvaa suruali za vitambaa.”



Hapo utakuwa umemwambia ukweli wako, kukubaliana na wewe au kukataa kutatokana na mapenzi yenu wewe na yeye. Kama anakupenda atakusikiliza. Kwani anamfurahisha nani huko barabarani zaidi yako? Kuwa mkweli.



UTARATIBU WA KAZI

Suala la kazi kwa baadhi ya wanandoa huwa ni tatizo. Utakuta mwanaume amemkuta binti wa watu anafanya kazi, wamependana na kufunga ndoa. Ghafla anamwambia mwenzake aache kazi!



Ndoa nyingi hasa changa huingia kwenye mgogoro huu. Kwangu mimi, wanandoa wote kufanya kazi ni bora zaidi, maana ile maana ya usaidizi wa mwanamke inakuwa imekamilika. Kwa maisha ya sasa mama kukaa nyumbani siyo ‘dili’ tena.



Hata hivyo, ili kuepusha matatizo, suala hili ni vyema mkajadiliana mapema. Kaa na mwenzako, mwulize: “Lakini dady, vipi kuhusu kazi baada ya kufunga ndoa?”



Anzisha huu mjadala na mwisho muwe na majibu yenye usawa. Mkubaliane kwa pamoja. Vijana wa mtaani wanasema, ‘kwa roho safi’. Hii itakusaidia maana mgogoro huu utakuwa umeisha kabla hata ya ndoa yenu.





VIPI NDUGU ZAKE?



Kama ni kweli una matarajio mazuri kutoka kwa mwenzako, kipengele hiki ni muhimu kabla ya kufanya uamuzi wa kuingia kwenye ndoa.



Lazima uijue vizuri familia yake. Anatoka katika familia ya namna gani? Kabila gani? Ukiachana na hilo, hapa lazima ufahamiane na ndugu zake, japo kidogo na upate muda wa kuwazoea.



Kuna familia nyingine ni wakorofi, kama ukiolewa huko ni tabu tupu. Pengine ukiona katika familia yao, labda wana tabia ya udokozi...si ajabu ukaibiwa hata wewe.

Kweli umempenda na unataka kuishi naye, lakini utaratibu mbaya wa ndugu zake ni kielelezo cha matarajio ya maisha yenu ya ndoa. Kuwa makini.



UNAIJUA AFYA YAKE?



Baadhi ya watu kwa bahati mbaya wana matatizo ya kiafya ya kudumu. Utakuta huyu ana udhaifu wa kusumbuliwa na shinikizo la damu, mwingine vidonda vya tumbo, kifafa n.k.



Ni udhaifu ambao yeyote anaweza kuwa nao. Kwa nini nimegusia hili? Kuna baadhi ya rafiki zangu wanaingia kwenye ndoa wakiwa hawajui matatizo ya wenzao, hivyo kusababisha usumbufu.



Hujui mwenzako anasumbuliwa na nini, mnagombana kidogo unaanza kumpiga, unashangaa ameanguka chini, damu zinaanza kumiminika puani! Si kosa lako, maana hukujua!



Hapa kuna umuhimu mkubwa sana wa kujua afya ya mwenzako. Kama ana maradhi ya kudumu ni vyema ukajua, ili pia ufahamu utakavyotakiwa kuishi naye ndani ya ndoa. Hakikisha unaijua historia ya afya yake vyema. Hakuna maana mbaya kufahamu, isipokuwa utakuwa na uwezo wa kumchukulia kulingana na udhaifu wake.



MILA NA DESTURI



Kuna makabila mengi nchini, kila watu wana mila zao, lazima uzijue japo kwa ufupi. Unaweza kuzungumza naye au ukawashirikisha watu wazima ambao wana ufahamu mkubwa, watakusaidia.



Unaweza kuingia kwenye kabila ambalo mila zake zinaruhusu mwanaume kulala na shemeji yake kama kaka yake hayupo; itakuwaje hapo kama ulikuwa hujui?



Kuna mengi ambayo siwezi kuyaandika yote, lakini jambo kubwa na muhimu kwako hapa ni kuhakikisha unafahamu mila na desturi za mume/ mke wako mtarajiwa.



KUHUSU IMANI ZA DINI



Inapendeza zaidi kama mkioana ndani ya imani moja ya dini. Upo utararibu wa wachumba kufunga ndoa bomani, ambapo kila mmoja huwa na dini yake. Siku za hivi karibuni wengi wanafanya hivyo, lakini si sahihi kwa asilimia mia moja.



Ndoa imara, ukiacha juhudi za wahusika wenyewe hujengwa na hulindwa na imani thabiti ya dini ya wahusika. Mnapokuwa katika imani moja, ni rahisi kumfikia Mungu pamoja katika maombi au kwenda kwa viongozi wa dini pamoja na kupewa ushauri wa kiroho.

Jambo hili lisiwe la mwisho, kama tayari dalili za kuoana zinaonekana wazi, muanze kujadiliana mapema juu ya suala la dini. Lazima muwe dhehebu moja, kama mpo tofuati, mshauriane ili mmoja amfuate mwenzake. Hakuna kinachoshindikana kwenye mazungumzo.



MNIE MAMOJA



Hapa namaanisha kwamba, ili ndoa yenu iwe bora lazima kuanzia mapema muwe na nia moja kwa kila jambo. Sina lugha nyepesi sana ya kudadavua hili, lakini kikubwa ni kwamba mnapaswa kuwa na mawazo ya aina moja kwa maana ya kushirikishana tangu mapema.

Jengeni mazoea ya kushirikishana kila kitu. Hii itawajengea uaminifu na kila mmoja kujiona sehemu ya mwenzake.



Kwa nini yote hayo?

Ndiyo taswira ya kile unachokiendelea ndani ya ndoa. Ikiwa uhusiano wenu awali haukuzingatia niliyoyataja hapo juu, matarajio ya ndoa yako yatakuwa kinyume.



Acha utaratibu wa kuamini kwamba kwenye ndoa kuna furaha, kuna starehe tu, kuna kusaidiana tu. Zipo changamoto ambazo lazima ukubaliane nazo au ujiandae kukutana nazo kuanzia mapema.



Kwa hakika hayo yakifuatwa kwa makini, ndoa yenu itakuwa bora na bila shaka utakuwa na matarajio mema katika ndoa yako ijayo.
CHANGIA MTAZAMO NA MAONI YAKO JUU YA HII MADA..
Facebook Comments Plugin Enhanced by Dira la mahusiano FB page