KABILA GANI ZURI LA KUOA/KUOLEWA? TUSHILIKIANE

 
Sijajua kwa nini nimeamua kuandika mada hii, ila nimejikuta tu nikiandika. Lakini nina sababu ambayo nadhani inatosha kukushawishi hata wewe tukajiuliza kwa pamoja. Nimewahi kukutana sana na swali hili na baadhi ya watu wakilizungumzia kwa namna ya kukebehi, kukejeli, kusifu na kuponda baadhi ya makabila linapofika suala la uhusiano wa kimapenzi au maisha ya ndoa.
“Umeoa Mmachame?, umekwisha, hao watu wabaya sana aisee, hawaoni taabu kukuua warithi mali,” mtu mmoja alimshangaa mwenzake baada ya kumwambia kuwa mwanandoa mwenzake anatokea Kilimanjaro katika kabila hilo.
“Hao Wangoni bwana, wape hela watafikisha, lakini mwanamke hafiki aisee, wahuni sana hao,” mwanamke mmoja alimweleza shoga yake baada ya kumtaarifu kwamba anajiandaa kufunga ndoa na mchumba wake ambaye ni Mngoni kutoka Ruvuma.
“Unaishi na Mhaya? Duh, mtawezana kweli, maana hao jamaa wana majivuno?!” mwingine naye anamshangaa mwenzake.

Kwa jumla, katika jamii yetu, tunalo tatizo hili kwa kiwango kikubwa sana, tukibaguana kwa misingi ya dini, kabila, elimu na vitu vingine chungu mzima. Tumeacha kuzungumzia mapenzi kwa maana ya uhusiano, tumeangukia katika kujadili vitu ambavyo havihusiki kabisa.
Rafiki yangu mmoja aliniambia kwamba alilazimika kuomba ushauri kwa watu wazima na majirani, ili aweze kushusha presha ya mama yake ambaye alikataa katakata mpango wake wa kuoa mwanamke anayetokea katika kabila la Warangi, wanaotokea Kondoa mkoani Dodoma, kwa sababu ambazo hazikumtosheleza hata kidogo.
Aliniambia kuwa mama yake alimweleza kuwa wanawake wa kabila hilo ni watu wanaopenda sana kutumia ushirikina katika uhusiano au ndoa zao.
Nimesikia mazungumzo ya namna hii kwa miaka mingi, nimejaribu kuchunguza kwa kuulizauliza watu wa makabila tofauti walio katika uhusiano na hata kusoma baadhi ya tafiti, inaonyesha kuwa hakuna ukweli wowote katika mapenzi yanayohusiana na tabia za kabila.
Hakuna uhusiano wowote kwa mfano, majivuno ya Mhaya na jinsi atakavyoishi kimapenzi na mwanamke ambaye wako kabila tofauti. Ni kweli, kwa nje, inaonekana kama hawa jamaa ni watu wa majivuni, lakini niwe mkweli kuwa ninao marafiki wengi Wahaya, lakini hawana majivuno hata kidogo.
Umalaya, ujivuni, ushirikina, uroho wa mali na vitu vingine, ni tabia binafsi ya mtu. Kulisingizia kabila ni kutotenda haki kwa sababu kwa mfano, wakati tukiambiwa kuwa wanaume wa Kingoni ni watu wa wanawake sana, upo ushahidi wa wazi kwamba Ruvuma si miongoni mwa mikoa yenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya gonjwa hatari la Ukimwi!
Mtu anapaswa kufanya uamuzi wa kuingia katika uhusiano wa kimapenzi na mtu kwa kufuata hisia zake na jinsi mwenyewe anavyomchukulia mwenza wake. Kuchagua kabila kama ndicho kigezo cha kuishi katika uhusiano ni ubaguzi, kitu ambacho ni dhambi kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
Wengi wameshangazwa na kuimarika kwa uhusiano wao ambao awali ulitiliwa mashaka na watu wengi. Wazee wetu vijijini wangependa tuoe au kuolewa na watu wa kabila letu, lakini katika dunia inayojikusanya kwa kiwango kikubwa na kuwa kijiji, fikra hizi zimepitwa na wakati.
Kitu cha msingi ni kuangalia na kuzifanyia kazi sifa unazozitaka kutoka kwa mpenzi wako. Kama ana upungufu, mchukulie yeye kama yeye na siyo kabila, dini au elimu yake. Mapenzi ni sanaa, ambayo ndani yake haina ukabila, usomi wala imani!
CHANGIA MTAZAMO NA MAONI YAKO JUU YA HII MADA..
Facebook Comments Plugin Enhanced by Dira la mahusiano FB page