Ukiona dalili za kwamba ni tapeli wa mapenzi, usimng’ang’anie eti tu kwa sababu umekufa kwake, muache!
NDUGU zangu, katika mapenzi wapo ambao wameingia kwenye ndoa na wenza ambao ni pasua kichwa. Unamkuta mwanaume kaoa mwanamke ambaye anaonesha dhahiri ni mapepe au mwanamke anaoa mwanaume kiwembe.
Katika mazingira haya ndoa lazima iwe chungu na kufuatiliana sana kutakuwa hakuepukiki kabisa. Aidha, naomba niseme tu kwamba, haipendezi kuwa na mwenza ambaye anakufanya umfuatilie kila mara kwa sababu unahisi anakusaliti.
Kufuatiliana, kuchunguzana kwa wanandoa kwa kweli haipendezi, ninachoona mimi ni kwamba, kama humuamini bora umuache kuliko kujipa kazi ya kumfuatilia kila wakati badala ya kufanya mambo mengine ya msingi.
Tutambue katika maisha ya ndoa kuna kitu kuridhika. Unapokuwa na mtu anayekupa kila aina ya furaha maishani mwako bila kuonesha tabia zinazokutia mashaka juu ya penzi lake, muamini halafu usiwaze kama anaweza kukufanyia yale ambayo yatakuumiza.
Ukiona dalili za kwamba ni tapeli wa mapenzi, usimng’ang’anie eti tu kwa sababu umekufa kwake, muache! Nasema muache kwa sababu, kutokuwa muaminifu ni ishara kwamba hana mapenzi ya dhati kwako na ukiendelea naye atakupa kazi ya wewe kumchunga, una muda huo?
Yaani na ugumu wa maisha ulivyo bado utumie muda wako ambao ungeutumia kufanya kazi kuanza kumuwekea mitego mkeo au mumeo eti ili umfumanie, ya nini yote hayo?
Hivi ukishamfumania utapata nini? Kwamba utakuwa umemuaibisha! Mimi sidhani kama kuna sababu ya kufikia huko.
Wapo ambao waliwawekea mitego wenza wao na walipowafumania, walipata presha na kujikuta wanafariki dunia na kumuacha mgoni akiendelea kujilia vyake. Itaumaje?
Mbaya zaidi baadhi ya watu wakifumaniwa huanza kuanika upungufu wa wenza wao. Utamsikia mwanamke akisema; “Mapenzi gani unayonipa, waache wenzako wanaojua mahaba na kutunza wafaidi. Mwanaume gani huwezi kuvaa, mwanaume gani mbahili, siwezi kukaa na mwanaume suruali…”
Hayo ni baadhi ya maneno ya shombo ambayo baadhi ya wanaume wamekuwa wakiambiwa na wake zao baada ya kuwafumania. Hivi kama inakutokea wewe utajisikiaje? Najua utaumia sana.
Ndugu zangu, tuna mambo mengi ya kufanya katika maisha yetu. Tusiyape nafasi mapenzi yatutibulie furaha kisha yatufanye tushindwe kufanya mambo ya msingi.
Ifike wakati tuone kwamba inapofika muda wa kuingia kwenye ndoa, tunawapa nafasi wale ambao tuna uhakika watatuongezea furaha badala ya kutufanya tujute.
Kama tutaoa bila kuangalia mtu mwenye tabia nzuri bali kwa kuvutiwa na mwanamke mzuri, aliyefungashia ambaye kila mwanaume atatamani awe wake, tujiweke tayari kupata ‘stress’ zinazoweza kutufanya tutakosa furaha kwenye ndoa.
Mwisho naomba niseme kwamba, huna sababu ya kuanza kumfuatilia mke/mume wako baada ya kubaini hajatulia. Utajipata vidonda vya tumbo bure.
Facebook Comments Plugin Enhanced by Dira la mahusiano FB page