JE UNAITAFUTAJE SURUHU BAADA YA KUKOMBANA NA MPENZI WAKO.?

 
HAKUNA binadamu aliyekamilika chini ya jua. Hayupo mtu ambaye hajawahi kukosea, hakosei na mwenye uhakika kuwa katika maisha yake yajayo hatakosea. Hayupo!
Marafiki zangu, nakwenda kuzungumzia kitu kikubwa sana ambacho ni sehemu ya maisha ya uhusiano. Ni kipengele kigumu zaidi kuliko vyote katika mapenzi. Upo kwenye ndoa au uhusiano, lakini kwa bahati mbaya, mwenzako ameteleza na kukukosea.
Wakati mwingine inaweza kuwa kosa kubwa kabisa ambalo si ajabu mkakaa hata mwezi mzima bila kuzungumza! Hapa kama hakutatumika busara ni wazi kuwa uhusiano wenu utakuwa upo hatarini.
Sehemu hii ndiyo ya kuonesha ukomavu wako katika uhusiano. Ukomavu ni pamoja na kufahamu namna ya kumaliza migogoro pindi inapotokea. Kwa bahati mbaya, mikwaruzano husafisha moyo. Hasira hutawala na wakati mwingine inaweza kusababisha kujichukulia uamuzi ambao baadaye unageuka majuto.
Marafiki zangu, hakuna ambaye hajawahi kugombana na mpenzi wake. Hata wewe unayesoma hapa inawezekana jana tu umemkwaza mwenzako. Jambo la msingi kwako ni kujua namna ya kumaliza matatizo yenu kwa njia salama na kukuacha mwenye amani zaidi katika penzi lenu.
Katika mada hii, nitafafanua njia kuu mbili za kumaliza matatizo ndani ya uhusiano, halafu mwisho utaona ni njia gani bora zaidi. Njia hizo ni kumaliza mgogoro mwenyewe, ya pili ni ile ya kuwashirikisha wengine.

NI SAHIHI KUWASHIRIKISHA WENGINE?
Kuna watu wana utaratibu wa kumaliza migogoro yao kwa kuwashirikisha watu wengine. Hapa sasa itategemea na ukaribu lakini wengi hukaa na watu wa karibu kama marafiki zao.
Ukiachana na hao, kuna wengine hufikisha ugomvi wao kwa wazazi wa upande mmoja au kwa mshenga. Wapo wanaosema kwamba si njia nzuri kuwashirikisha watu wa pembeni kwenye ugomvi wa ndani, mawazo yao yana ukweli kwa namna fulani, lakini hapa nitafafanua zaidi.
Marafiki, hakuna ubaya kuwashirikisha watu wa karibu ili kuwasuluhisha. Pamoja na hivyo, kuna mipaka, kwa maana ya kwamba aina ya ugomvi na namna mlivyoshindwa kuelewana ninyi kwa ninyi.
Mathalani, si vizuri kuwashirikisha wazazi katika ugomvi mdogo wa kawaida kama wa ‘huyu mwanamke kidomodomo sana!’ au ‘janaume lenyewe vivu, halikidhi haja yangu’.

Haya ni mambo madogo sana ambayo hayahitaji hata rafiki wa karibu kujua kinachoendelea. Ni jambo la kukaa ninyi wenyewe na kuelezana. Kikubwa ni namna mnavyoelezana. Mnatumia kauli gani, utulivu upo kwa kiasi gani n.k.
Kimsingi jambo la wazazi kufahamu lazima liwe kubwa sana, ambalo pia umeshalipigia kelele mara nyingi, lakini mwenzako haelewi, sasa hapo unaweza kuamua kuwashirikisha wazazi ili muweze kuchota busara zao.

Kuna ugomvi wa kati ambao si vibaya kuwashirisha marafiki zenu. Kikubwa kwako ni kuangalia rafiki ambaye ni muelewa na anayeheshimiana sana na huyo unayekwenda kumshtakia. Ngazi inayofuata baada ya hapo ni ndugu wa karibu, nikimaanisha dada, kaka, mashemeji au mawifi.
Si kila kitu kukimbiza kwa wazazi, hawa wenyewe wataingia katika hatua ya pili baada ya kujiridhirisha kwamba rafiki zenu wa karibu wameshindwa kumaliza tatizo lenu.

KWA NINI WENGI HUKIMBILIA KWA WENGINE?
Zipo sababu nyingi lakini kubwa ni kukimbia majukumu au hasira za kupindukia. Kubwa zaidi ni namna mhusika anavyomheshimu mwenzake. Kwa maneno mengine, ukiona mwenzako anakwenda kuomba marafiki zake wawakukutanishe ili mzungumzie matatizo yenu, maana yake anaamini unamdharau!
Hili ndiyo kubwa kuliko, yaani kwa vile anajua unamdharau, anahofia hata akikuelekeza kwa namna gani hutaelewa, utakuwa mkaidi na mbishi na usiyetaka kuelekezwa. Mhusika huamua kuchukua hatua hiyo pia, kwa lengo la kuepusha ugomvi zaidi.
Anaamini kwa kuzungumza peke yenu (kwa kuwa anaamini unadharau), utamjibu majibu ya hovyo na si ajabu ukaibuka mgogoro mpya. Kwa sababu anakupenda na hataki kukupoteza, anaamini kwa kupitia marafiki zake/wako unaweza kuelewa zaidi na uhusiano wenu ukaendelea.

FAIDA ZA KUWASHIRIKISHA
Hakuna chenye faida kikakosa kuwa na hasara, katika pande zote mbili kuna faida na hasara zake, hebu tukaone katika kipengele hiki kabla ya kumalizia kipengele kilichobaki.
(a) Ni rahisi kudhibiti hasira
Kikao cha usuluhishi wa wapenzi kilichowashirikisha watu wengine kinatawaliwa na amani. Kila mmoja hupewa haki ya kuzungumza kile anachoona amekosewa na kutoa pendekezo la namna ya kumaliza tatizo husika.
Si rahisi kukuta wakizungumza kwa sauti ya juu au jazba, maana kila mmoja anaamini anafuatiliwa kwa karibu na wasuluhishi wao, hivyo kuonesha hasira, ingemtafsirisha kwamba yeye ndiye mkorofi namba moja!

(b) Humaliza matatizo kwa haraka
Kwa namna yoyote ile ni ukweli kwamba, kwa kuwashirikisha marafiki matatizo huzungumzwa kwa uwazi, huku mifano hai ikitolewa na hivyo kuwafanya wahusika kuelewa kwa haraka na kukubaliana na makosa, kisha kusameheana.

(c) Aibu ya kurudia kosa
Kumaliza ugomvi mbele ya kikao, kunaongeza umakini kwa aliyekosea. Kunamuimarisha na kumkomaza, lakini pia hawezi kukubali kuonekana mpumbavu kwa kurudia kosa lile lile. Kwanza atachunga kutorudia kosa, lakini itampa aibu kufanya kosa jingine kwa hofu ya kukutanishwa tena kwenye kikao.
Nafasi yangu ni ndogo, kwa leo naomba niishie hapa. Wiki ijayo tutaona hasara za kuwashirikisha marafiki. Naweka kituo kikubwa.
CHANGIA MTAZAMO NA MAONI YAKO JUU YA HII MADA..
Facebook Comments Plugin Enhanced by Dira la mahusiano FB page