Msomaji wangu, nataka kuzungumzia mada ambayo huenda ikawaweka wengi katika njia panda na kushindwa kufanya maamuzi sahihi linapokuja suala la kutafuta mpenzi sahihi.
Katika maisha ya binadamu kuna kupenda na waswahili wanasema, kupenda ni upofu. Unaweza kumpenda mtu fulani watu wakakushangaa na kuuliza umempendea nini, lakini ndiyo hivyo moyo wako umeishapenda.
Ila sasa kitu ambacho nataka kukizungumza leo ni kuhusu kumjua mtu vilivyo kabla ya kuingia naye katika uhusiano wa kimapenzi. Wapo niliojaribu kuongea nao juu ya hili lakini asalimia kubwa wakasema eti unapotokea kumpenda mtu fulani haina haja kuijua historia yake lakini wapo pia waliosema kuwa, ili kuwa na uhusiano wenye mwanga ni vizuri kujua upande wa pili wa huyo uliyetokea kumpenda.
Mimi naungana na hawa wanaosema kuna umuhimu wa kuijua angalao kwa ufupi historia ya mtu ambaye umempenda. Nasema hivyo kwa kurejea historia ya binti mmoja aliyekuwa anaitwa Zainabu. Alikuwa ni binti mzuri kiumbile na kisura. Alizaliwa Dar na kukulia maeneo ya Magomeni Kagera.
Msichana huyu alikuwa akiwachanganya sana wanaume na kila alikopita alitongozwa hadi akaona kero. Awali alikuwa na msimamo wa kutokuwa tayari kuchezewa na mwanaume yeyote, lililokuwa moyoni mwake ni kumpata mwanaume mwenye mapenzi ya dhati kwake ili amuoe lakini wakati akiwa na umri wa miaka 18 alianza kuishiwa nguvu ya kukabiliana na vishawishi, akaanza kujiachia!
Akawa hakamatiki, alilala na kila mwanaume aliyemshobokea hasa waliokuwa na vijisenti. Kimsingi aliingia kwenye kundi la wasichana malaya. Hakuna mwanaume mkware pale mtaani ambaye hakumuonja na mbaya zaidi, kila aliyekuwa akitembea naye alijiona mwenye bahati kwa kuwa wa pekee kwa msichana huyo, baada ya mapenzi ndipo walipogundua kumbe kwa wakati huo Zai alikuwa si chochote.
Kilichokuja kikiwachanganya wanaume wengi pale mtaani ilikuwa baada ya taarifa ya kuwa Zai aliwahi kutembea na pedeshee mmoja ambaye ni muathirika. Pale mtaani wanaume wakaanza kumgwaya binti huyo, hakuna aliyepata nguvu tena ya kumtongoza na kila aliyetembea naye alihisi naye tayari kaambukizwa. Wengi wakaanza kuishi kwa matumaini hata kabla ya kwenda kupima.
Cha ajabu Zai ndiyo kwanza alikuwa akizidi kuwa na mvuto wa ajabu. Alipoona mambo yameharibika pale mtaani, akahamia Arusha. Huko nako aliendeleza mchezo wake huo huo wa kubadili wanaume, wapo waliofikia hatua ya kutangaza ndoa bila hata kujua huko alikotoka ilikuwaje?
Wengi hawakuwa na haja kujua historia yake, walivutiwa na muonekano wake tu. Wanaume wakafikia hatua ya kupigana kumgombea. Wakati huo binti huyo alikuwa kipesa zaidi, waliokuwa na kisu kikali ndiyo waliobahatika kula nyama. Zai akawa anakula vichwa kama hana akili nzuri lakini siku ya siku, akaanza kuumwa! Bila hata kwenda kupima na kujua kinachomsumbua, akajua tayari ameshaukwaa.Ukweli ilikuwa kwamba binti huyo alishaathirika!
Baada ya kuona hivyo akaamua kumrudia Mungu huku muonekano wake ukiwa vile vile. Hakuonekana mgonjwa, usoni mwake hapakuwa na alama kwamba alikuwa malaya huko nyuma lakini kwa pale mtaani wanaume wakaanza kumgwaya. Waliokuwa wakiendelea kudata naye walikuwa wale wasiomjua na wakati huo ndiyo akawa sasa na msimamo kwamba, anataka mwanaume wa kuoa.
Mara akakutana na Kassim kijana ambaye alivutiwa sana na Sophy na bila hata kuuliza pale mtaani tabia za binti huyo akatangaza ndoa.
Sikujua mwisho wa wawili hao lakini naamini hadi hapo utakuwa umepata picha ya kwamba Kassim kampapatikia msichana ambaye hakuijua historia yake vizuri na kujikuta akitangaza ndoa kwa binti aliyeamini kuwa ni mtu aliyetulia kumbe….!
Mpenzi msomaji wangu, wapo ambao katika maisha yao wamekuwa wakitumia ule msemo usemao, bata ukimchunguza sana huwezi kumla. Kwa kutumia msemo huo wamekuwa hawazingatii umuhimu wa kumchunguza mtu kabla ya kuanzisha uhusiano naye.
Ninachoweza kusema ni kwamba, ni kweli bata ukimchunguza sana huwezi kumla lakini pia iweje ukubali kuuziwa mbuzi kwenye gunia?
Yaani kweli leo leo unakutana na mvulana ambaye hujui alikotokea alikuwa na uhusiano na nani na waliachana kwa sababu gani, wewe unaanza kumshobokea na kuanzisha uhusiano naye? Huko siyo kujitafutia matatizo kweli? Je, kama mwanaume huyo ni jambazi?
Hivi hadi hapo huoni tu kwamba kuna ulazima wa angalau kujua kidogo historia ya mtu husika kabla ya kuingia kichwa kichwa? Kinachotakiwa ni kuwa na moyo wa kupuuza baadhi ya mambo utakayoyasikia kuhusu yeye.
Kwa mfano, unaambiwa alishawahi kutembea na watu kumi, hiyo siyo ‘ishu’ sana na inabaki kuwa historia, kikubwa ni kwamba akiwa na wewe atatulia? Hatakuwa na tamaa tamaa za kijinga? Wapo wasichana ambao huko nyuma walikuwa malaya wa kutupwa lakini wamepata wanaume waliowaonesha kuwapenda na wakaolewa.
Sasa ndoa zao hazina matatizo kabisa, kwanini? Kwa sababu waliamua kubadilika na kuachana na mambo ya kijinga. Hiyo inaonesha kuwa historia mbaya ya mtu haiwezi kukufanya ukashindwa kumpenda.
Pointi ya msingi ni kwamba, ni bora ukajua kwamba huyo uliyenaye huko alikotoka alikuwa mwingi wa habari na kuanzia hapo ujue namna ya kumbadilisha kuliko kuwa na mtu ambaye ikifika hatua ya kukuonesha uhalisia wake atakuchanganya na kukuharibia mfumo mzima wa maisha yako.
Facebook Comments Plugin Enhanced by Dira la mahusiano FB page