Kuna watu wana kawaida ya kuzikataa sifa walizonazo na kutaka kuwabebesha wengine. Mathalan, wewe ni mbishi sana na ubishi wako umekuwa ukisababisha malumbano yasiyokwisha kwa mwenzi wako. Hutapata ufumbuzi kama hutajitambua, ukijikataa ni mzigo wako mwenyewe na utakutesa kila siku.
Wakati mwingine ni kazi ngumu kujitambua lakini itakupa unafuu mkubwa kama utakapofanikiwa huo mtihani. Utaepukana na mzigo wa kuwalaumu wengine, utajikuta upo huru kuliko ambavyo unaweza kuwaza na kupata jibu hivi sasa. Lifanyie kazi suala hili kwa mafanikio yako ya baadaye.
Wala haitakuumiza na ukidhamiria ni kitu rahisi. Wakati ujao, likitokea tatizo la aina yoyote, kabla hujamshushia lawama mwenzako, angalia ukweli uliopo ndani yako. Je, hakuna kosa la upande wako? Jibu utakalopata ndilo ambalo litakuwezesha kuingia kwenye dunia ya furaha na mapenzi yenye utamu na siyo mateso.
CHAGUA MAPAMBANO
Huwezi kuanzisha uhusiano halafu moja kwa moja mambo yakawa tambarare. Kuna mambo ambayo lazima uyafanyie kazi. Hayo ndiyo nayaita mapambano. Ukishachagua mapambano, moja kwa moja utaelewa namna ya kujipanga ili kushinda hayo mapambano ambayo umejichagulia.
Wanasema maisha ni vita, kwa hiyo ili kushinda lazima upambane. Kwa maana hiyo, wakati mwingine furaha haiji hivihivi. Unatakiwa kuijenga na wakati mwingine unaanza kwa kuitafuta. Jukumu ulilonalo ni kuhakikisha unawekeza nyenzo halisi za mapambano yako kuhakikisha mapenzi yanakuwa matamu.
Mfano; Umemkuta mwenzi wako akiwa na tabia ambazo hazikufurahishi. Je, tabia hizo ni zipi? Ukishajua kile kinachomsumbua mwenzi wako, bila shaka hapo utakuwa umeshabaini kile ambacho unatakiwa kupambana nacho. Hatua inayofuata ni kuamua mbinu za kushughulikia tatizo.
Wakati mwingine, mwenzi wako ni mgogoro mtindo mmoja. Kila kitu unachoweza kufanya kinaweza kuibua malumbano. Ukimuuliza kitu, badala ya kukujibu yataibuka mabishano. Ukimkosoa kwa chochote ni maneno juu ya mikwaruzano. Hapo kazi unayo, kuinua mikono juu ni njia mojawapo lakini kupambana mpaka ushinde ni jambo lingine.
Wapo wale ambao, hata pongezi kwao inaweza kuibua malumbano. Mfano, unamwambia mwenzi wako umependeza, badala ya kukujibu asante, anaweza kukuuliza: “Kwani siku nyingine huwa sipendezi.” Ukimjibu huwa anapendeza, atakuhoji ni kwa nini huwa humsifii, badala yake umemsifia siku hiyo.
Pengine badala ya kupokea pongezi, yeye akajibu: “Ni kawaida yangu.” Vilevile, inawezekana akakuhoji maswali mpaka ukakoma siku nyingine kumpongeza kwa kupendeza. Hayo ni mambo ambayo unapaswa kuamua ama kuyarekebisha au kuyakimbia kama utakuwa unataka furaha katika uhusiano wako wa kimapenzi.
Huo ni mfano tu lakini angalizo kwako ni kwamba uamuzi wa kukimbia ni sawa lakini huyo ambaye utakutana naye ni binadamu, naye utamkuta ana kasoro zake, kwa hiyo utatakiwa uamue kuainisha upoungufu alionao kabla ya kuchagua mapambano na mbinu za kupambana. Usikimbie, hebu tulia na ufanye juu chini kumbadilisha.
Hata hivyo, wakati ukimbadilisha jaribu kujiuliza maswali ambayo yana msaada mkubwa sana kwako unapoyapatia majibu. Ainisha vitu vinavyokukwaza kwa mwenzi wako halafu jiulize kabla hujaingia rasmi kwenye mapambano ya kuyaondoa hayo mambo yanayokukwaza ili uyafurahie mapenzi yako.
Kuna maswali matatu ya kujiuliza. Haya kama dira yako lakini kama unadhani yapo mambo mengine ambayo yanajitokeza kwenye uhusiano wako na unapaswa kujiuliza na kupata majibu kwa haraka.
Facebook Comments Plugin Enhanced by Dira la mahusiano FB page