Hizi ndo mbinu za kuishi na mpenzi wako na kudumisha mahusiano yenu mhimu kujua
Hata
kama utapinga haya, lakini ukweli utabaki pale pale; Kila jinsia
inahitaji sana kuungana na jinsia nyingine katika tendo muhimu na la
kihistoria katika maisha liitwalo ndoa! Yes, huu ni ukweli ambao upo
wazi na utaendelea kusimama kama ulivyo.
Jinsia zote zina umuhimu na jambo hili muhimu, lakini kuna tofauti kidogo, kwamba mwanamke
anasubiri kufuatwa na
mwanaume, wakati mwanaume anaamua kumfuata mwanamke anayemtaka na kwa
wakati wake. Kuna kitu nataka kuweka sawa hapa, kwamba wanaume ndiyo
huwa wa kwanza kupenda kabla ya mwanamke, ingawa mwanamke anaweza kuwa
wa kwanza kupenda lakini akashindwa kufikisha hisia zake kwa mwanaume
husika.
Wanawake wa ‘mjini’ huwa hawakubaliani na hili, kutokana
na huu utandawazi unaohubiriwa siku hizi ikiwa ni pamoja na kampeni za
usawa zinazotetewa na Wanaharakati Wanawake. Akina dada nao huchangamkia
kueleza hisia zao kwa wanaume. Nadhani si jambo baya, ingawa linaweza
kupokelewa kwa hisia tofauti na kila mwanaume.
Tuyaache hayo,
hoja kubwa ya msingi hapa ni jinsi gani mwanamke anaweza kuolewa haraka
na mpenzi wake. Ikumbukwe kwamba, hapa nazungumza na wanawake ambao
tayari wapo katika uhusiano, lakini wenzi wao hawana habari kabisa na
mambo ya ndoa.
Katika matoleo yaliyopita, niliwahi kuzungumza kuhusu
namna gani mwanamke anaweza kuwashawishi wanaume wakataka kuingia katika
uhusiano naye. Leo nazungumzia juu ya wewe ambaye upo katika uhusiano
ambao haueleweki, lakini ndoa unaitaka. Unajua cha kufanya? Fuatana
nami.
EPUKA MAKUNDI HATARI
Mwanaume anapenda kuwa na mke
mwenye staha, ambaye hana tabia za hovyo. Kuwa na makundi ya
‘mashangingi’ ni alama ya kwanza kabisa kuwa unapenda au tayari una
tabia za kishangingi. Wanaume wengi hawapendi kabisa wanawake wenye
tabia za hovyo, wenye kampani ambazo si nzuri.
Lakini yawezekana,
jamaa alishakuambia juu ya kilio chake hiki, lakini wewe umekuwa kama
umeweka pamba masikioni mwako, hili ni tatizo. Linda heshima yako, kaa
mbali na makundi hatari, ili umfanye jamaa akuone wewe ni mwanamke
thabiti ambaye huigi, hushabikii na wala huna tabia mbaya. Utaonesha
hili kwa kukaa mbali na makundi ya wanawake hatari! Umenipata?
ZINGATIA MAVAZI YAKO
Kila
mtu anamjua mtu wake alivyo, mwanamke hata wewe unamjua mpenzi wako
alivyo. Sina shaka unafahamu anapenda nini na nini anachukia. Unajua
kabisa, nina uhakika na hilo. Lakini pamoja na kwamba jamaa anaweza kuwa
na vitu ambavyo vinamvutia zaidi, hata wewe kama mtoto wa kike, una
mapendekezo yako au vitu ambavyo unapenda zaidi kuvifanya!
Huzuiwi,
lakini swali la msingi, mwenzi wako anapenda? Kama wewe unapenda sana
skin jeans na top inayoacha kitovu nje, yeye hapendi kwa sababu ana nia
ya kukufanya mke hapo baadaye. Sasa utakuwa mke gani ambaye hata Salim
anaona sehemu zako za faragha hadharani?
Ukiachana na chaguo la
mwenzi wako, lakini lazima wewe mwenyewe kama mwanamke wa mtu,
ujitambue! Jisitiri vyema. Kwani kuna urembo gani wa kuvaa nguo
inayoonesha mwili wako ulivyo? Kuna burudani gani kuacha nyeti zako
wazi? Unataka nani akuone ulivyo? Mke hana sifa hiyo dada yangu, sasa
ili uweze kuwa na sifa hii muhimu, lazima uzingatie sana mavazi yako.
JIPE MOYO
Hili
nilishawahi kulizungumza sana katika mada zilizopita, baadhi ya
wanawake wamekuwa wakikatishwa tamaa na rafiki zao au watu wengine
wanaowazunguka, eti hawana hadhi ya kuolewa au watahangaika sana lakini
hawatapata mume, kisa eti HAVUTII!
Mwingine anajinyima mwenyewe
nafasi akisema; “Mimi nina balaa, sina bahati ya kuolewa, ndiyo maana
wadogo zangu wote wameolewa nimebaki mimi.”
Huu ni uvivu wa kuwaza. Lakini dada yangu, habari iliyo njema kwako ni kwamba, ndoa unaitengeneza wewe mwenyewe.
Unaitengeneza
kwa misingi ya kwanza, kujipa moyo mwenyewe kwamba wewe ni mzuri na una
sifa na haki za kuolewa kama wanawake wengine. Jipe moyo mwenyewe, huna
nuksi wala balaa, wewe ni mzuri na una sifa za kuwa mke hapo baadaye.
Iko
hivi, ukianza kujishusha mwenyewe, ni dhahiri kwamba hata mavazi yako
hayatakuwa mazuri, uso wako hautakuwa na tabasamu na wala hutakuwa na
matumani moyoni, hapo sasa ni mwanzo wa kuzorota afya yako. Utapata
mchumba kweli? Utasubiri sana kwa mtindo huo.
ACHA PAPARA
Haizuiwi
kuuliza kuhusu mustakabali wa uchumba wenu, lakini ni vizuri basi kuwa
na kiasi. Kuuliza kila wakati au kuwa mtu wa kulaumu, hakutakusaidia
kumfanya jamaa achukue maamuzi ya haraka ya kukuoa na badala yake
yanaweza kumpa picha tofauti.
Ni rahisi kuwaza kwamba, unachohitaji
kwake ni ndoa na baada ya hapo hutakuwa na staha tena. Kuwa mjanja,
achana na papara. Usilogwe ukamfanyia jambo zuri mpenzi wako, halafu
ndiyo umuulize; “Sasa honey, mbona hata huzungumzii ndoa yetu? Hivi
utanioa kweli? Eeeh baby? Niambie basi mpenzi wangu...”